Uchanganuzi wa Ufaafu wa Tafsiri ya Ombi la Baba Yetu kutoka Kiingereza hadi Kiswahili
Keywords:
Makala Asili, Makala Lengwa, Tafsiri, Udhaifu, UfaafuAbstract
Makala hii ilichunguza ufaafu wa tafsiri ya ombi la Baba Yetu kutoka Kiingereza hadi Kiswahili. Watafiti wanashikilia kuwa tafsiri inafaa kuwa na ufanifu mkubwa kuliko udhaifu. Lengo la watafiti ni kudhihirisha ufaafu na udhaifu wa tafsiri hii. Sanaa ya tafsiri ni muhimu sana katika ulimwengu wa sasa. Imewezesha mawasiliano ya kimataifa hasa katika elimu, biashara na shughuli za kidiplomasia. Watafiti wanakubali kuwa mchakato wa tafsiri huathiriwa na vizuizi kama vile vya kitamaduni na kimuktadha na hata tofauti za kisarufi katika lugha tofauti. Katika makala hii, matini asili na matini lengwa zilisomwa, vipengele vya ufaafu na udhaifu kudondolewa kisha watafiti kutoa msimamo wao wakiongozwa na mkabala wa House (1977 & 2015) kuhusu ubora wa tafsiri na pia nadharia ya Tafsiri ya Kimawasiliano ya Newmark. Walipata matokeo ya utafiti huu kama kuhifadhiwa kwa maana katika matini lengwa. Usawa wa kikazi unaopendekezwa na House ulidhihirika na pia usawa wa kimawasiliano unaozungumziwa na Newmark ulijitokeza. Utafiti huu utakuwa wenye manufaa kwa wanafunzi, wahadhiri na wasomi wengine katika uwanja wa tafsiri kwa vile utakuwa rejeleo muhimu katika kazi za tafsiri. Kwa kufanya hivi, watafiti wanaamini kuwa tafsiri sahihi ni kichocheo katika mafanikio ya mawasiliano.